Wanachama 6 wa Ikhwanul Muslimin wauawa nchini Misri
(last modified Wed, 25 Sep 2019 07:46:47 GMT )
Sep 25, 2019 07:46 UTC
  • Wanachama 6 wa Ikhwanul Muslimin wauawa nchini Misri

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imetangaza kuwa, polisi wa nchi hiyo wamewapiga risasi na kuwaua wanachama sita wa Ikhwanul Muslim katika mapigano yaliyotokea baina ya pande hizo mbili.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imesema kuwa, mapigano ya silaha yametokea baina ya wanachama wa Ikhwanul Muslimin na polisi katika mji wa "6th of October" ulioko kusini magharibi mwa Cairo na kupelekea wanachama 6 wa Ikhwanul Muslimin kuuawa.

Wizara hiyo imedai pia kwenye taarifa yake hiyo kwamba, wanachama hao wa Ikhwanul Muslimin walikuwa na nia ya kufanya opereseheni za kigaidi nchini Misri.

Polisi wa Misri

 

Mwaka 2013, serikali ya Misri ilitangaza kuwa Ikhwanul Muslimin ni miongoni mwa makundi ya kigaidi. Tangazo hilo lilikuja baada ya jeshi la Misri kumpindua rais wa kwanza wa nchi hiyo kuchaguliwa kidemokrasia, Mohammad Morsi ambaye alikuwa mwanachama wa Ikhwanul Muslimin. 

Mahakama ya kusikiliza kesi za jinai ya Misri, mara kwa mara  imekuwa ikiwahukumu viongozi wa Ikhwanul Muslimin kwa jicho hilo hilo la ugaidi.

Miongoni mwa tuhuma walizobebeshwa viongozi hao wa Ikhwanul Muslimin huko Misri ni kufanya ujasusi, kufichua nyaraka za siri kwa madhara ya usalama wa taifa, kushirikiana na makundi yenye silaha ya ndani na nje ya Misri ili kufanya ugaidi, kuvamia jela na kushirikiana na askari wa kigeni pamoja na kuharibu mali za umma.

Tags