Mamia ya watoto waliokuwa wakishikiliwa mateka Nigeria waokolewa
Jeshi la Polisi la Nigeria limetangaza habari ya kuwakomboa watu 300, aghalabu yao wakiwa watoto wadogo, ambao walikuwa wameshikwa mateka ndani ya jengo moja katika mji wa Kaduna, kaskazini mwa nchi.
Yakubu Sabo, Msemaji wa Jeshi la Polisi mjini Kaduna jana Ijumaa aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa, aghalabu ya mateka hao ni vijana wadogo wa kuanzia na umri wa miaka mitano.
Amesema karibu vijana wote waliokombolewa wamepatikana wamefungwa minyororo miguuni. Haijabainika wamekuwa katika jengo hilo kwa muda gani.
Msemaji wa Polisi katika mji wa Kaduna ameongeza kuwa, vijana wawili miongoni mwao ni raia wa Burkina Faso na kwamba waliosalia ni wakazi wa maeneo ya kaskazini mwa Nigeria.
Ripoti zinasema kuwa, mateka hao wana alama za kuonyesha kuwa waliteswa, kuachwa njaa kwa vipindi virefu na hata kunajisiwa.
Baadhi ya wazazi wa watoto hao wameviambia vyombo vya usalama kuwa watoto hao walikuwa katika taasisi ya elimu ya dini, ingawaje hawaelewi ni kwa nini walikuwa wamewekwa chini ya mazingira magumu hivyo.
Hivi karibuni Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ulisema tokea mwaka 2013 hadi sasa, magaidi wa Boko Haram wamewateka nyara maelfu ya watoto wadogo katika maeneo ya kaskazkini na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.