Kikao cha AU, UN kuhusu vita dhidi ya ugaidi Somalia
Maafisa wa ngazi za juu wa Tume ya Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM na Umoja wa Mataifa wamekutana Jumatatu mjini Mogadishu ili kubaini ramani ya njia ya kurefusha muda wa shughuli na operesheni za AMISOM kutoka mwaka 2019 hadi 2021.
Katika taarifa, AMISOM imesema mkutano huo wa ngazi ya juu unalenga kuratibu shughuli na operesheni zake nchini Somalia. Kwa mujibu wa mkuu wa AMISOM Fransisco Madeira, mkutano huo umeandaliwa katika wakati ambao tume hiyo inafanya kazi muhimu kabisa kama vile operesheni endelevu za kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shabaab, kuimarisha usalama katika njia kuu na pia kulinda usalama wa maeneo ya raia.
Mkutano huo wa siku tano unawaleta pamoja maofisa kutoka makao makuu ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, wawakilishi wote wa majeshi na polisi wa nchi zinazoshiriki na maofisa wa ngazi za juu wa AMISON kutoka jeshi, polisi na sekta za kiraia.
Wanajeshi wa AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone. Nao maafisa wa polisi wa AMISOM ni kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.
AMISOM ina askari wapatao 21,000 nchini Somalia ambao wanalinda amani katika nchi hiyo inayosumbuliwa na vita vya ndani kwa robo karne sasa.
Somalia ambayo inahesabiwa kuwa moja ya nchi masikini zaidi duniani imekuwa ikikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tokea mwaka 1991 kipindi ambacho Siad Barre aliyekuwa rais wa nchi hiyo alingólewa madarakani.