Spika wa Bunge Misri amfananisha Rais wa nchi hiyo na Adolf Hitler
Spika wa Bunge la Misri amemfananisha Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi hiyo na dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolf Hitler.
Hatua hiyo ya Spika wa Bunge la Misri imekuja baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kumtaja mwenzake wa Misri, Abdel Fattah al Sisi kuwa ni dikteta anayempenda sana.
Spika wa Bunge la Misri Ali Abdel Aal Sayyed Ahmed amemuunga mkono rais wa nchi hiyo akimfananisha na dikteta wa zamani wa Ujerumani na kusema kuwa, japokuwa Adolf Hitler alifanya makosa mengi lakini ndiye sababu ya maendeleo yanayoshuhudiwa sasa nchini Ujerumani.
Akihutubia Bunge la Misri Jumatano ya jana, Ali Abdel Aal alipongeza kazi zinazofanywa na serikali ya al Sisi na kusema Misri inahitajia hatua ngumu kama ilivyokuwa Ujerumani ya kipindi cha Hitler.
Matamshi hayo ya Spika wa Bunge la Misri yamezusha mjadala mkubwa baina ya raia wa nchi hiyo ambayo wiki za hivi karibuni imekumbwa na maandamano makubwa ya wananchi wanaomtaka Abdel Fattah al Sisi ang'atuke madarakani. Maandamano hayo yanafanyika kutokana na wito wa Muhammad Ali anayeishi uhamishoni nchini Uhispania ambaye ni miongoni mwa wapinzani wakubwa wa serikali ya al Sisi.
Kabla ya kukimbilia nje ya nchi, Muhammad Ali alikuwa mkandarasi wa jeshi la Misri na amefichua jinsi kiongozi wa sasa wa nchi hiyo anavyopora mali ya umma na kujitajirisha yeye, familia na majenerali wa jeshi kwa kujenga majumba na masri ya kifahari.
Hivi karibuni Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International pi lilikosoa vikali ukandamizaji na kamatakamata dhidi ya waandamanaji nchini Misri na kusisitiza kuwa nchi hiyo imekuwa gereza kubwa la wakosoaji wa serikali.