16 waaga dunia baada ya kufukiwa kwenye mgodi wa dhahabu DRC
Wachimba migodi 16 wamefariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa dhahabu huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Auguy Musafiri, Gavana wa mkoa wa Maniema mashariki mwa DRC amesema ajali hiyo ilitokea jana Jumatano katika mgodi wa Kampene, na kwamba makumi ya watu wanahofiwa kupoteza maisha.
Hata hivyo amesisitiza kuwa, kufikia sasa wamefanikia kupata miili 16 kutoka kwenye maporomoko hayo na kwamba shughuli za kusaka miili zaidi zinaendelea.
Stéphane Kamundala, mwanaharakati wa kijamii katika eneo hilo amesema mgodi huo haramu ulikuwa na wafanyakazi zaidi ya 20.
Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya wachimba migodi zaidi ya 50 kufariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi haramu wa dhahabu nchini Chad.
Kadhalika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, watu 43 waliaga dunia katika maporomoko mengine yaliyotokea kwenye mgodi wa dhahabu unaosimamiwa na kampuni ya Glencore yenye makao makuu yake mjini Baar nchini Uswisi.
Takwimu zinaonyesha, aghalabu ya madini hususan ya dhahabu na almasi yanayochimbwa kinyume cha sheria Kongo DR, Chad miongoni mwa nchi nyingine za Afrika, husafirishwa kimagendo katika nchi za Ulaya na Uarabuni.