Misri: Mazungumzo yetu na Ethiopia kuhusu bwawa la al-Nahdhah yamevunjika
(last modified Sun, 06 Oct 2019 08:13:13 GMT )
Oct 06, 2019 08:13 UTC
  • Misri: Mazungumzo yetu na Ethiopia kuhusu bwawa la al-Nahdhah yamevunjika

Serikali ya Misri imesema mazungumzo mapya kati ya nchi hiyo na Ethiopia kuhusu bwawa la al-Nahdhah linalojengwa na Addis Ababa yamegonga mwamba.

Taarifa iliyotolewa hapo jana na Wizara ya Maji na Kilimo cha Unyunyizaji ya Misri baada ya mazungumzo ya nchi mbili hizo pamoja na Sudan mjini Khartoum imesema, "Mazungumzo yamevunjika kutokana na ukwamishaji mambo wa Ethiopia."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, serikali ya Cairo inakaribisha kwa mikono miwili upatanishi wa kimataifa, baada ya duru kadhaa za mazungumzo ya pande mbili kutozaa matunda. 

Ethiopia na Misri zimefanya vikao mbalimbali kuhusu mradi wa bwawa la al-Nahdhah ambalo gharama ya ujenzi wake inafika dola bilioni 4; hata hivyo hadi sasa bado hakujafikiwa muafaka licha ya kupigwa baadhi ya hatua.

Bwawa la Nahdha la Ethiopia (Grand Renaissance Dam)

Serikali ya Misri imekuwa ikisisitiza kuwa ujenzi wa bwawa hilo unapunguza kiwango cha maji yanayoingia nchini humo kutokea kwenye miinuko ya Sudan.

Mwezi Aprili mwaka 2011 Ethiopia ilianza ujenzi wa bwawa hilo kuu ambao ulitazamiwa kumalizika hadi kufikia mwaka 2015, hata hivyo hadi sasa ujenzi huo haujamalizika bali umefikia karibu asilimia 63. Bwawa hilo linatajwa kuwa mradi mkubwa zaidi wa uzalishaji umeme kutokana na maji ya Mto Nile barani Afrika. 

Tags