UNICEF: Surua yaua watu 4000 DRC, ni hatari zaidi ya Ebola
Watu wasiopungua 4,000 wamepoteza maisha kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Surua (measles) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC huku hali ikiripotiwa kuendelea kuwa mbaya.
Hivi sasa mashirika ya Umoja wa Mataifa yanatekeleza mpango maalumu wa kuwapatia chanjo watoto zaidi na kupeleka huko dawa za kuokoa maisha.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kupitia taarifa yake iliyotolewa Jumatano inasema watu 4,000 wamepoteza maisha tangu mwezi Januari mwaka huu na kwamba idadi hiyo ni kati ya wagonjwa 203,179 walioripotiwa kwenye majimbo yote 26 ya taifa hilo.
Cha kusikitisha zaidi ni kuwa, asilimia 74 ya wagonjwa hao wa surua ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na mbaya zaidi ni kuwa, takribani asilimia 90 ya vifo ni watoto wa umri huo.
Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC, Edouard Beigbeder amesema idadi ya wagonjwa wa surua nchini humo mwaka huu ni mara tatu zaidi ya wagonjwa walioripotiwa mwaka 2018 akisema kuwa surua umekuwa ugonjwa hatari zaidi kuliko Ebola ambayo tangu mwezi Agosti mwaka jana hadi leo hii umesababisha vifo vya watu 2,143.
Beigbeder amesema kwa ushirikiano na serikali na wadau, UNICEF imeongeza kasi ya utoaji wa chanjo kwa watoto na wakati huo huo kunazipatia kliniki dawa za kutibu dalili za ugonjwa huo.
Tayari serikali ya DRC inajiandaa kuzindua awamu ya pili ya kampeni ya chanjo tarehe 22 mwezi huu wa Oktoba, ambayo inalenga kuwapatia watoto wenye umri kuanzia miezi 6 hadi miaka mitano katika majimbo yote 26 chanjo dhidi surua.