Magaidi 11 wa al-Shabaab wauawa na jeshi la Somalia wakikusanya ushuru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56656-magaidi_11_wa_al_shabaab_wauawa_na_jeshi_la_somalia_wakikusanya_ushuru
Askari wa Jeshi la Taifa la Somalia wamefanikiwa kuwaangamiza wanachama 11 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab katika operesheni ya jana Jumanne kwenye eneo la Gedo, kusini mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 16, 2019 04:12 UTC
  • Magaidi 11 wa al-Shabaab wauawa na jeshi la Somalia wakikusanya ushuru

Askari wa Jeshi la Taifa la Somalia wamefanikiwa kuwaangamiza wanachama 11 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab katika operesheni ya jana Jumanne kwenye eneo la Gedo, kusini mwa nchi.

Ali Muhammed Hassan, Kamanda wa Kikosi cha 49 cha jeshi la Somalia amesema wanajeshi wa serikali walifanya operesheni hiyo nje ya mji wa Bardhere, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wakazi wa mji huo kuhusu harakati za al-Shabaab.

Amesema maafisa usalama wamefanikiwa kuokoa mifugo 300 waliokuwa wamechukuliwa kwa nguvu na magaidi hao kutoka kwa wakazi wa mji huo.

Ameongeza kuwa, wanajeshi wa serikali wamewatia mbaroni wanachama kadhaa wa genge hilo kufuatia operesheni hiyo, na kwamba wengine wametoroka wakiwa na majeraha ya risasi.

Wakazi mji wa Bardhere, kusini mwa Somalia wamekuwa wakihangaishwa na al-Shabaab kwa muda sasa

Wakazi hao wamesema wanachama hao wa genge la ukufurishaji wamekuwa wakiwasumbua wakazi hao kwa kuwaitisha ushuru na kodi kwa nguvu.

Hivi karibuni, wazee wanane wa vijiji vya eneo la Galmudug nchini Somalia waliuawa kwa kukatwa vichwa na kundi moja la wanamgambo lenye mfungamano na al-Shabaab, eti kwa kukataa kulipa kodi na 'zaka'.