Nigeria: Hakuna fedha za kutosha kwa ajili ya kupambana na Boko Haram
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ulinzi ya Bunge la Nigeria ametangaza kuwa, serikali ya nchi hiyo haina fedha za kutosha kwa ajili ya kugharamia mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram
Mohammed Ali Ndume amesema kuwa, utafiti uliofanywa na kamisheni hiyo umebaini kwamba, jinai zinazofanywa na wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi katika nchini Nigeria na katika nchi nyingine jirani ni kubwa sana kiasi kwamba bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kuweka mikakati ya kitaifa na kimataifa ya kusitisha jinai hizo haitoshi.
Afisa huyo wa Nigeria amekanusha uvumi unaodai kuwa, Nigeria imetenga bajeti ya Naira bilioni 100 kwa ajili ya masuala ya ulinzi mwaka 2020 na kusema: Nigeria iko vitani na kwamba hata kama serikali ingetenga kiwango hicho cha fedha basi kisingetosha kwa ajili ya kukabiliana kundi hilo la kigaidi.
Kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo limekuwa likifanya jinai za kutisha katika nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika hususan Nigeria lilitangaza kuungana na makundi ya kigaidi ya Daesh na al Qaida.
Kundi hilo limeua watu zaidi ya elfu 50 na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi tangu lilipoanzisha mashambulizi nchini Nigeria na nchi kadhaa jirani mwaka 2009.