Libya yahamishia nchini Misri wahamiaji haramu 95
Serikali ya Libya imewahamishia nchini Misri makumi ya wahamiaji haramu wanaodaiwa kuwa na magonjwa ya kuambukiza.
Idara ya Kusimamia Uhamiaji katika mji wa mashariki wa Benghazi nchini Libya imeripoti kuwa, wahamiaji haramu 95 wamepelekwa nchini Misri kwa kutumia usafiri wa mabasi.
Siku ya Jumatatu, idara hiyo iliwahamishia katika nchi za Nigeria na Misri wahamiaji haramu wengine zaidi ya 100.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limeripoti kuwa, kuna wakimbizi na wahamiaji haramu 650,000 nchini Libya, ambapo 6,000 miongoni mwao wakiwemo wanawake na watoto wadogo wanazuiliwa katika vituo mbalimbali.
Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Rwanda imewapokea wakimbizi 189 kutoka Libya kufikia sasa.
Serikali ya Rwanda imesema iko tayari kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi 30,000 kutoka Libya lakini itawakaribisha kwa utaratibu maalumu na katika hatua kadhaa, ili kuzuia nchi hiyo yenye watu milioni 12 isiwe na mzigo.