Oct 20, 2019 02:34 UTC
  • Jeshi la Mali laua magaidi 50 katika operesheni ya kulipiza kisasi

Kwa akali magaidi 50 wameuawa katika operesheni ya kulipiza kisasi ya Jeshi la Mali katikati ya nchi.

Taarifa ya Jeshi la Mali inasema kuwa, operesheni hiyo ya askari wa nchi hiyo imepelekea kujeruhiwa magaidi 30, kuharibiwa silaha zao mbali na kunusuru wanajeshi 36 kati ya 60 wa nchi hiyo waliokuwa wametekwa nyara na magaidi hao katika mashambulizi ya mwishoni mwa mwezi uliopita wa Septemba.

Kundi moja la kigaidi lilishambulia kambi mbili za jeshi la Mali Septemba 30, ambapo askari 38 wa serikali waliuawa na makumi ya wengine kushikwa mateka.

Aidha mapema mwezi huu, Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani nchini Mali (MINUSMA) kilitangaza habari ya kuuawa askari wake watano katika mripuko wa bomu uliotokea kwenye eneo la Aguelhok, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Moja ya magenge ya kigaidi nchini Mali

Kwa miezi kadhaa sasa maeneo ya kaskazini na katikati mwa Mali yamekuwa uwanja wa machafuko na mashambulizi ya makundi yenye silaha.

Mwaka 2012 jeshi la Mali lilifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoing'oa madarakani serikali ya kiraia. Tangu wakati huo hadi hivi sasa machafuko yameikumba nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika hususan katika maeneo ya kaskazini na katikati mwa nchi.

Tags