Polisi ya Nigeria yakomboa 'wanafunzi' wengine 150 Kaduna
Polisi nchini Nigeria kwa mara nyingine tena imefanikiwa kuwaokoa watoto na vijana mabarobaro wapatao 150 kutoka katika kituo kimoja ambako walikuwa wakifanyiwa mateso kaskazini mwa nchi.
Katika operesheni hiyo ya jana Jumamosi, maafisa usalama walivamia kituo hicho cha mateso ambacho kilikuwa kinadaiwa ni cha kutoa mafundisho ya dini na kuokoa watoto na vijana 150.
Gavana wa jimbo la Kaduna, Nasir El Rufai aliagiza kufanywa msako dhidi ya kituo hicho kilichoko katika mji wa Rigasa, na kuokoa watoto waliokuwa wanazuiliwa na kuteswa humo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita pia, maafisa usalama katika jimbo la Kaduna la kaskazini mwa Nigeria walitangaza kuwa, vikosi vya usalama vimefanikiwa kugundua shule moja katika jimbo hilo na kuwaokoa watoto na mabarobaro 500 waliokuwa wakiteswa kwa njia mbalimbali kwa ajili ya malengo maalumu.
Operesheni ya jana ni ya nne iliyofanywa katika eneo la kaskazini mwa Nigeria, ambapo hadi sasa watoto na vijana zaidi ya elfu moja wamekombolewa. Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa, vijana hao walikuwa wakiteswa vikali kimwili, kisaikolojia na hata kunajisiwa.
Akthari ya wahanga hao ni Wanigeria huku wengine wakiwa ni raia kutoka katika nchi jirani za Burkina Faso, Mali na Ghana na walipelekwa katika vituo hivyo na watu wasiojulikana au wazazi wao kwa ahadi ya kwenda kusoma masomo ya dini.