Ajali ya basi nchini DRC yaua watu 30
Watu wasiopungua 30 wamefariki dunia huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya basi walimokuwa wakisafiria kuteketea moto.
Kwa mujibu wa taarifa ajali hiyo ilijiri Jumapili karibu na eneo la Mbanza-Ngungu kusini magharibi mwa mji mkuu Kinshasa.
Imearifiwa kuwa basi hilo lilipata ajali wakati likiwa linasafiri kutoka mji wa Lufu ullio katika mpaka wa nchi hiyo na Angola likielekea Kinshasa kabla ya kuteketea moto.
Afisa wa utawala katika eneo la Mbanza-Ngungu Didier Nsimba amesema ajali hiyo ilitokea baada ya breki za basi hilo kufeli. Inashukiwa kuwa basi hilo ambalo lilikuwa limebeba abiria kupita kiasi lilikuwa limesheheni mzigo wa petroli ambayo ilichangia kuenea moto haraka.
Maafisa wa usalama wanasema basi hilo lilikuwa na abiria 100 wakati wa ajali na mili iliyotetektea haiwezi kutambulika. Eneo la Mbanza-Ngungu liko umbali wa kilomita 150 kutoka Kinshasa na hushuhudia ajali mbaya mara kwa mara. Idadi kubwa ya watu hupoteza maisha barabarani kila mwezi nchini DRC kutokana na kupindukia kasi, magari mabovu, kubeba abiria na mizigo ziada na hali mbaya ya barabara.