Mwito wa utulivu baada ya watu 16 kuuawa katika maandamano Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56823-mwito_wa_utulivu_baada_ya_watu_16_kuuawa_katika_maandamano_ethiopia
Jawar Mohammed, mwanaharakati na mwasisi wa mtandano huru wa vyombo vya habari nchini Ethiopia ametoa mwito wa utulivu baada ya watu 16 kuuawa katika machafuko na ghasia za maandamano nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 24, 2019 12:51 UTC
  • Mwito wa utulivu baada ya watu 16 kuuawa katika maandamano Ethiopia

Jawar Mohammed, mwanaharakati na mwasisi wa mtandano huru wa vyombo vya habari nchini Ethiopia ametoa mwito wa utulivu baada ya watu 16 kuuawa katika machafuko na ghasia za maandamano nchini humo.

Wafuasi wa mwanaharakati huyo tangu juzi Jumanne jioni wamekuwa wakishiriki maandamano katika mji mkuu Addis Ababa dhidi ya Waziri Mkuu, Abiy Ahmed na hivyo kutia doa Tuzo ya Amani ya Nobel ambayo alishinda hivi karibuni.

Watu 16 wameripotiwa kuuawa katika makabiliano baina ya waandamanaji hao na maafisa usalama katika mji mkuu na miji mingine, huku makumi ya wengine wakijeruhiwa.

Mwanaharakati huyo amewataka wafuasi wake wafungue barabara walizofunga, waondoe vizuizi walivyokuwa wameweka barabarani, wawatibu waliojeruhiwa kwenye machafuko hayo sambamba na kusuluhisha mgogoro uliopo.

Jawar Mohammed ambaye mwaka jana aliitisha na kuongoza maandamano yaliyomleta madarakani Abiy Ahmed, anaituhumu serikali ya Waziri Mkuu huyo kuwa inapanga njama ya kumuua na kwamba tayari imeshampokonya walinzi wake.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed

Hii ni katika hali ambayo, Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema taifa hilo liko tayari kwa uchaguzi mkuu ambao umepangwa kufanyika mwezi Mei mwaka ujao. 

Uchaguzi huo mkuu utakuwa wa kwanza kufanyika Ethiopia chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliyeingia madarakani mwezi Aprili mwaka jana na kuanza kutekeleza mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.