UN: Nchi za Pembe ya Afrika zinahitaji misaada baada ya mafuriko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56949-un_nchi_za_pembe_ya_afrika_zinahitaji_misaada_baada_ya_mafuriko
Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi za Pembe ya Afrika katika miezi michache iliyopita zimesababisha mafuriko na mahitaji ya misaada ya kibinadamu hususan nchini Ethiopia, Sudan Kusini na Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 30, 2019 08:12 UTC
  • UN: Nchi za Pembe ya Afrika zinahitaji misaada baada ya mafuriko

Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi za Pembe ya Afrika katika miezi michache iliyopita zimesababisha mafuriko na mahitaji ya misaada ya kibinadamu hususan nchini Ethiopia, Sudan Kusini na Somalia.

Katika taarifa, Jens Laerke msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA, imesema nchini Ethiopia, mafuriko yameripotiwa katika maeneo ya Afar, Amhara, Gambela, Oromia, SNNP na Somali huku yakifurusha watu 220,000 na kusababisha uharibifu wa mali na vyanzo vya kipato. Takriban watu nusu milioni kwa ujumla wameathiriwa na mafuriko ya hivi majuzi.

Ameongeza kuwa, nchini Sudan Kusini, mafuriko ya msimu tangu Julai yameathiri zaidi ya watu 900,000 wakiwemo wakimbizi wa ndani, wakimbizi na jamii zinazowahifadhi huku mvua zikitarajiwa kuendelea kwa wiki zingine nne au sita na huenda zikahatarisha maisha ya watu wengine.

Mafuriko nchini Tanzania

Nchini Tanzania idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mvua inakadiriwa kuwa 40 na katika nchi jirani ya Kenya watu takribani 30 nao pia wamepoteza maisha kufuatia mafuriko.