Magaidi 32 waaangamizwa katika operesheni mbili tofauti nchini Burkina Faso
Jeshi la Burkina Faso limetangaza kuwa, limewaua kwa akali magaidi 32 katika operesheni mbili tofauti kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Taarifa ya jeshi la Burkina Faso imeeleza kwamba, magaidi 24 waliuawa katika operesheni ya kwanza siku ya Ijumaa na kwamba, magaidi wengine wanane waliuawa katika operesheni ya pili siku ya Jumamosi.
Duru za jeshi la Bukina Faso zinasema kuwa, mwanajeshi mmoja ameuawa pia katika operesheni hizo dhidi ya magaidi.
Aidha idadi kadhaa ya wanawake waliokuwa wakishikiliwa mateka na kutumiwa katika utumwa wa ngono na magaidi hao wamekombolewa kufuatia operesheni hizo.
Operesheni hizo za jeshi la Burkina Faso zinafanyika siku chache baada ya watu wasiopungua 37 kuuawa katika shambulio la kundi la wabeba silaha dhidi ya mgodi wa dhahabu kaskazini mwa nchi hiyo.
Mapema mwezi uliopita wa Oktoba, watu wasiojulikana walivamia mgodi mwingine wa dhahabu katika kijiji cha Madudaji katika mkoa wa Sam kaskazini mwa nchi na kuua makumi ya watu.
Aidha mwishoni mwa mwezi uliopita, watu wengine 16 waliuawa katika kile kinachosadikiwa kuwa ni shambulizi la kigaidi kaskazini mwa nchi.
Tangu mwaka 2015 hadi hivi sasa, magenge ya kigaidi yameongeza mashambulizi yao katika maeneo mbalimbali hasa ya kaskazini na mashariki mwa Burkina Faso. Hadi hivi sasa watu wasiopungua 600 wameshauawa kwenye mashambulio hayo.