Afrika Kusini yasitisha uuzaji silaha kwa Saudia, UAE
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57445-afrika_kusini_yasitisha_uuzaji_silaha_kwa_saudia_uae
Afrika Kusini imetangaza kuwa inasitisha uuzaji wa silaha zake kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) baada ya kubainika kuwa tawala hizo mbili zinawakabidhi wanamgambo wa Yemen baadhi ya silaha hizo na hivyo kukiuka mapatano ambayo yanazuia silaha zilizonunuliwa kutoka Afrika Kusini kufikia pande za tatu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 23, 2019 11:57 UTC
  • Afrika Kusini yasitisha uuzaji silaha kwa Saudia, UAE

Afrika Kusini imetangaza kuwa inasitisha uuzaji wa silaha zake kwa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) baada ya kubainika kuwa tawala hizo mbili zinawakabidhi wanamgambo wa Yemen baadhi ya silaha hizo na hivyo kukiuka mapatano ambayo yanazuia silaha zilizonunuliwa kutoka Afrika Kusini kufikia pande za tatu.

Shirika la habari la Reuters limewanukulu maafisa wanne ambao hawakutaka majina yao kutajwa na barua za siri na kuandika kuwa, sababu nyingine ya hatua hiyo ni kuwa, kwa mujibu wa kipingee katika mapatano ya uuzaji silaha, wanunuzi wa kigeni  wa silaha wanapaswa kuwaruhusu maafisa wa Afrika Kusini kukagua vituo vyao vya kijeshi. Hata hivyo Saudia na UAE ambazo hununua takribani asilimia 30 ya silaha zote za Afrika Kusini zinazouzwa nje ya nchi zimekataa vituo vyao vikaguliwe kwa madai kuwa huo ni ukiukwaji wa mamlaka yao ya kujitawala.

Ezra Jele, Mkurugenzi wa udhibiti wa silaha za kawaida katika Wizara ya Ulinzi ya Afrika Kusini amesema nchi yake huzingatia vigezo vya haki za binadamu, mapigano ya kieneo, hatari ya silaha kupewa wengine, maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na maslahi ya taifa wakati wa kuchunguza vibali vya uuzaji nje silaha.

Watoto ni kati ya waathirika wakuu wa hujuma ya Saudia na vibaraka wake dhidi ya Yemen

Saudia Arabia na waitifaki wake katika eneo, hasa UAE, walianzisha vita dhidi ya Yemen mnamo Machi 2015 kwa lengo la kuurejesha madarakni utawala wa kibaraka wao, Abd Rabbu Mansour Hadi, na kuitimua harakati ya Ansarullah ambayo imekuwa ikilisaidia Jeshi la Yemen katika kukabiliana na wavamizi. Hata hivyo hadi sasa Saudia haijaweza kufikia malengo yake hayo.

Mwezi Februari Televisheni ya CNN ilibaini kuwa silaha za Marekani ambazo zimeuziwa Saudia na UAE zimepatikana mikononi mwa wanagamabo nchini Yemen. Mwezi huo huo pia, Amnesty International ilichapisha ripoti iliyobaini kuwa silaha ambazo UAE imezinunua kutoka nchi za Magharibi na nchi zinginezo zimepatikana mikononi mwa wanamgamabo ambao wametenda jinai za kivita nchini Yemen.