Harakati ya Kiislamu ya Nigeria yasisitiza kukabiliana na vitisho vya serikali
Ofisi ya Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesisitiza katika ujumbe wake uliotuma kwamba watakabiliana ipasavyo na vitisho na hatua za serikali ya nchi hiyo.
Ofisi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeandika katika ujumbe wake uliotuma katika ukurasa wake wa Twitter kwamba viongozi wa serikali wanadhani kuwa wanaweza kufanya jambo lolote lile.
Ujumbe huo umeeleza kuwa kamwe madaraka hayawezi kutathminiwa kwa mujibu wa namna viongozi wa serikali ya Nigeria wanavyotumia silaha kukabiliana na wananchi bali yanapimwa kwa mujibu wa huduma zao kwa wananchi na kiwango cha uchungu walionao kwa watu wao.
Ofisi ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imetoa ripoti yake hiyo katika hali ambayo maafisa wa Idara ya Intelijinsia ya Nigeria wamekataa kumruhusu Sheikh Zakzaky kufanya mahojiano na waandishi habari.
Itakumbukwa kuwa, Sheikh Zakzaky na mkewe Agosti 12 mwaka huu walielekea India kwa ajili ya matibabu hata hivyo Agosti 14 waliondoka nchini humo na kuelekea NIgeria kutokana na kutoridhishwa na mchakato wa matibabu, kuwepo vizuizi vya kiusalama na kukosekana daktari mwenye kuaminika.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe wanaendelea kushikiliwa hadi hivi sasa tangu waliposhambuliwa na jeshi la Nigeria Disemba 13 mwaka 2015 katika Husseiniya katika mji wa Zaria nchini humo.