Shehena ya silaha kutoka Imarati yawasili nchini Libya
Duru za habari nchini Misri zimeelezea kuwasili nchini Libya shehena ya silaha kutoka Imarati.
Mtandao wa habari wa al-Arabi al-Jadid umevinukuu vyanzo vya habari nchini Misri vikisema kwamba shehena hiyo ya silaha imetumwa Libya kwenda kwa wanamgambo wa jenerali muasi Khalifa Haftar, ambao wanajiita 'jeshi la kitaifa la Libya.' Kwa mujibu wa duru hizo za habari, lengo la Abu Dhabi la kutuma silaha hizo ni kuliimarisha kundi hilo la wanamgambo hasa baada ya wapiganaji wa kundi hilo kushindwa hivi karibuni na jeshi la serikali ya maridhiano ya kitaifa. Siku chache baada ya kutumwa kwa shehena hiyo ya silaha, askari kadhaa wa Imarati kutoka Misri waliingia Libya kwa lengo la kutekeleza masuala yanayohusiana na operesheni za kijeshi na kutoa msaada wa kilojestiki kukiwemo kurusha angani ndege zisizo na rubani.
Kundi linalojiita jeshi la kitaifa la Libya chini ya uongozi wa Khalifa Haftar na ambalo kwa miaka kadhaa limekuwa likipata uungaji mkono kutoka Saudia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi hususan Marekani na waitifaki wake, na ambalo limekuwa likidhibiti eneo la mashariki mwa Libya, miezi michache iliyopita lilisonga mbele kuelekea kaskazini mwa nchi hiyo.