Maandamano yashtadi Algeria licha ya kutangazwa mshindi wa urais
Wananchi wa Algeria wameendelea kufanya maandamano katika barabara za miji mikubwa ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Algiers, licha ya mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni kutangazwa.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Abdelmadjid Tebboune ndiye mshindi wa uchaguzi huo kwa kupata asilimia 58.15 ya kura. Ni asilimia 40 tu ya Waalgeria zaidi ya milioni 24 waliotimiza masharti ya kupiga kura, walioshiriki zoezi hilo.
Waziri wa zamani wa utalii wa Algeria, Abdelkader Bengrine ameshika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 17.38 ya kura, akifuatiwa na Ali Benflis aliyekuwa waziri mkuu wa Algeria baina ya mwaka 2000 na 2003 aliyezoa asilimia 10.55.
Wagombea wanne kati ya watano wa uchaguzi huo wa rais wote wanadai kuwa ni washindi, wakisisitiza kwamba uchaguzi huo unapaswa kuingia duru ya pili.
Uchaguzi wa rais nchini Algeria ulifanyika Alkhamisi katika anga ya mzozo na mvutano mkubwa kutokana na wananchi wa nchi hiyo kugawanyika katika makundi mawili ya wanaopinga na wanaounga mkono kufanyika uchaguzi huo.
Waalgeria wengi wamesusia uchaguzi huo wakisema wagombea wote ni wanasiasa wenye mfungamano na utawala za rais wa zamani wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika unaohusishwa na ufisadi mkubwa na utendaji mbaya.