Tebboune aapishwa kuwa rais mpya wa Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57984-tebboune_aapishwa_kuwa_rais_mpya_wa_algeria
Abdelmajid Tebboune ameapishwa leo Alkhamisi kuwa rais wa Algeria, huku harakati ya upinzani ya Hirak ikiendelea kujadili ombi la kiongozi huyo la kufanya mazungumzo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 19, 2019 09:49 UTC
  • Tebboune aapishwa kuwa rais mpya wa Algeria

Abdelmajid Tebboune ameapishwa leo Alkhamisi kuwa rais wa Algeria, huku harakati ya upinzani ya Hirak ikiendelea kujadili ombi la kiongozi huyo la kufanya mazungumzo.

Tebboune amekula kiapo cha kulitumikia taifa katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Rais katika mji mkuu wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, Algiers.

Ameahidi kushughulikia changamoto za kisiasa, kijamii na kiuchumi zinazolikabili taifa hilo, sambamba na kufanya mazungumzo na makundi ya kisiasa na kijamii, ili kuiondoa nchi hiyo kwenye mgogoro unaoikabili kwa miezi kadhaa sasa.

Abdelmajid Tebboune mmoja wa mawaziri wakuu wa utawala wa Abdelaziz Bouteflika alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo baada ya kupata asilimia 58.15 ya kura. 

Maandamano ya kupinga uchaguzi Algeria

Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Algeria alitangaza kuwa, asilimia 41.13 ya wananchi walishiriki katika uchaguzi huo wa rais uliofanyika Alkhamisi ya wiki jana.

Uchaguzi huo ulikua wa kwanza wa rais kufanyika Algeria baada ya kuondoka madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika Aprili Pili mwaka huu. 

Miezi kadhaa kabla ya uchaguzi na hata siku ya uchaguzi wenyewe, baadhi ya wananchi wa Algeria walifanya maandamano ya kupinga zoezi hilo la kidemokrasia, wakidai kuwa wagombea wote wamewahi kuhudumu katika utawala wa Bouteflika.