Ripoti: Idadi ya watu waliofariki dunia kwa Ebola DRC imefikia 2,231
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58195-ripoti_idadi_ya_watu_waliofariki_dunia_kwa_ebola_drc_imefikia_2_231
Idadi ya watu waliofariki dunia kwa maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeongezeka na kufikia 2,231.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Dec 30, 2019 03:59 UTC
  • Ripoti: Idadi ya watu waliofariki dunia kwa Ebola DRC imefikia 2,231

Idadi ya watu waliofariki dunia kwa maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeongezeka na kufikia 2,231.

Hayo yamo katika ripoti mpya ya mashirika ya kimataifa yanayojishughulisha na kampeni za kukabiliana na maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ripoti hiyo inaeleza kwamba, watu 2,231 wamefariki dunia hadi sasa kwa maradhi ya Ebola kwenye kesi 3,373 za watu waliothibitishwa kukumbwa na maradhi hayo.  Ripoti hiyo imetolewa siku chache tu baada ya maafisa wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutangaza kuwa, maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola yameongezeka katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.

Hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa, lilikaribia mno kutokomeza maradhi ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), lakini kuibuka mapigano na machafuko kulivuruga na kukwamisha juhudi za kupambana na ugonjwa huo.

Daktati akimpatia chanjo  ya Ebola mmoja wa raia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Mripuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ulianza Mei 8 mwaka 2018 katika mji wa Bikoro mkoani Equater kaskazini magharibi mwa nchi na baadaye kuenea katika mji wa Mbandaka katikati mwa mkoa huo na pia mashariki mwa nchi hiyo.

Tangu mwaka 2014 hadi sasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeshakumbwa na miripuko mitatu ya ugonjwa wa ebola.

Kirusi cha ugonjwa huo hatari kimeshaua watu wapatao 11,000 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 katika maeneo mbali mbali duniani.