Baraza la Usalama la UN lalaani mripuko wa Mogadishu, Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58208-baraza_la_usalama_la_un_lalaani_mripuko_wa_mogadishu_somalia
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mripuko wa kigaidi uliotokea katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu na kuua makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 30, 2019 23:15 UTC
  • Baraza la Usalama la UN lalaani mripuko wa Mogadishu, Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mripuko wa kigaidi uliotokea katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu na kuua makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.

Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa tamko na sambamba na kulaani mripuko huo wa kigaidi wa Mogadishu limesema kuwa, magaidi wanaendelea kuhatarisha usalama na amani kote ulimwenguni.

Tamko hilo aidha limetaka kufuatiliwa na kutiwa mbaroni haraka wahusika wa mripuko huo likisisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa daima uko pamoja na serikali na wananchi wa Somalia na unaunga mkono juhudi zote za kuleta maendeleo, utulivu na ustawi nchini humo.

Kabla ya hapo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa naye alikuwa amelaani vikali shambulizi hilo la kigaidi lililotokea Jumamosi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na kuua makumi ya watu.

António Guterres alitoa tamko rasmi Jumamosi usiku na sambamba na kulaani shambulio hilo la kigaidi alielezea kusikitishwa mno na mripuko huo na alisema yuko pamoja na serikali na wananchi wa Somalia katika wakati huu mgumu. 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

 

Nchi nyingi duniani, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimelaani mripuko huo wa gari lililokuwa limeshehenezwa mabomu na kuua kigaidi zaidi ya watu 90 na kujeruhi wengine wengi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Ingawa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo, lakini kidole cha lawama kimeelekezwa kwa genge la ukufurishaji la al Shabab lililojitangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida. Genge hilo limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara kama hayo ndani na nje ya Somalia.

Genge la kigaidi la al Shabab liliundwa mwaka 2007 kwa shabaha ya kuipindua serikali kuu ya Somalia. Mwaka 2011 genge hilo la ukufurishaji lilitimuliwa katika maeneo mengi liliyokuwa linayadhibiti ukiwemo mji mkuu Mogadishu. Hata hivyo bado lina wafuasi wake katika vijiji vya mbali vya Somalia.