ADF yafanya shambulizi jingine na kuua watu 23 Kongo DR
Watu wasiopungua 23 wameuawa katika kijiji kimoja kilichoko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia mashambulio ya kundi la waasi la ADF la Uganda.
Maafisa wa eneo hilo pamoja na viongozi wa mashirika ya kutetea haki za binadamu walisema jana Jumatatu kuwa, shambulizi hilo lilitokea katika eneo lenye misitu mingi la Apetina, lililoko kilomita chache kutoka mpaka wa Uganda.
Donat Kibwana, mshirikishi wa eneo la Beni la mashariki mwa DRC amethibitisha kutokea hujuma hiyo na kuongeza kuwa, mbali na watu 23 kuuawa, nyumba kadhaa ziliteketezwa moto na waasi hao wa ADF.
Mapema mwezi huu, watu 22 waliuawa katika mji wa Beni wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulizi jingine la waasi wa ADF.
Katika miezi ya hivi karibuni, wanamgambo hao wa ADF ambao asili yao ni Uganda wamekuwa wakiwashambulia raia, maafisa usalama na hata maafisa wa afya wanaopambana na ugonjwa hatari wa Ebola, mashariki mwa nchi.
Hivi karibuni, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikiongezea muda wa mwaka mmoja mwingine kikosi cha kusimamia amani cha umoja huo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO, licha ya upinzani na malalamiko ya wananchi wa DRC wanaotaka askari hao kuondoka nchini humo kwa kushindwa kuwadhaminia usalama wao.