Mji mkuu wa Nigeria washuhudia mandamano ya kulaani kuuliwa kigaidi Jenerali Soleimani
Wakazi wa mji mkuu wa Nigeria, Abuja wamefanya maandamanao ya kulaani jinai ya Marekani ya kumuua kigaidi Meja Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH wakati akiwa safarini nchini Iraq.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria aidha imetoa tamko na mbali na kuilaani Marekani kwa kumuua kigaidi Kamanda Qassem Soleimani, imelipa mkono wa pole taifa na serikali ya Iran na kusisitiza kuwa, ugaidi huo wa Marekani ni jinai isiyosameheka.
Nchi, taasisi, vyama na shakhsia mbalimbali duniani wanaendelea kulaani jinai hiyo ya Marekani ya kumuua shahidi Meja Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds, cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, SEPAH.

Miongoni mwao ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uingereza, cha Leba, Jeremy Corbyn ambaye ametoa mwito kwa serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua za kukabiliana na vitendo vya kichokozi vya Marekani.
Meja Jenerali Qassem Solaimani na naibu wa mkuu wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq, al Hasdul Shaabi, Abu Mahdi al Muhandes waliuawa shahidi usiku wa kuamkia jana Ijumaa katika shambulizi la roketi lililofyatuliwa na helikopta ya Marekani katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani imetangaza kuwa, rais wa nchi hiyo Donald Trump ndiye aliyetoa amri ya kuuliwa shahidi Jenerali Qassem Soleimani na wote aliokuwa ameandamana nao.