UN: Somalia inahitaji msaada wa kibinadamu wa dola bilioni moja mwaka 2020
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58697-un_somalia_inahitaji_msaada_wa_kibinadamu_wa_dola_bilioni_moja_mwaka_2020
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, Somalia inahitaji msaada wa zaidi ya dola bilioni moja kwa ajili ya huduma za kibinadamu katika mwaka wa 2020.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2020 08:15 UTC
  • UN: Somalia inahitaji msaada wa kibinadamu wa dola bilioni moja mwaka 2020

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, Somalia inahitaji msaada wa zaidi ya dola bilioni moja kwa ajili ya huduma za kibinadamu katika mwaka wa 2020.

Kwa mujibu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM fedha hizo ni za kuwasaidia watu zaidi ya milioni 3 kwa mahitaji ya msingi ya kibinadamu,

Akizungumza baada ya kuzindua wito huo wa msaada uliofanyika mjini Moghadishu Somalia mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Adam Abdelmoula  amesema Somalia bado inaendelea kukabiliwa na matatizo makubwa ya kibinadamu. Ameongeza kuwa,  miezi michache tu iliyopita watu zaidi ya nusu milioni waliathirika na mafuriko ambayo yalikumba sehemu kubwa ya Somalia.

Uzinduzi huo wa Mpango wa Kukabiliana na Masuala ya Kibinadamu (HRP) wa jumla ya dola bilioni 1.03 umehudhuriwa pia na waziri wa Somalia wa masuala ya kibinadamu na udhibiti wa majanga Hamza Said Hamza aliyesema mpango huu unaashiria azma ya jamii ya kimataifa katika kuwasaidia watu wa Somalia.

Mafuriko nchini Somalia

Ameongeza kuwa mgogoro wa kibinadamu Somalia unachangiwa na vita vya miaka mingi, ukame wa muda mrefu , na bila shaka mafuriko yaliyoshuhudiwa mwaka 2019.

Fedha hizo za mpango wa HPR zitasaidia watu milioni 3 wakiwemo milioni 1.7 waliotawanywa na vita, kutokuwepo usalama, kuhamishwa kwa nguvu, ukame na mafuriko na msaada utakuwa katika mfumo wa mgao wa chakula, elimu, huduma za afya, maji safi na salama na pia ulinzi kwa walio katika hatari ya ukatili wa kijinsia.

UNSOM imesema mwaka huu mahitaji ya ufadhili ya mpango wa usaidizi wa kibinadamu yamepungua kwa asilimia 11 kutoka dola bilioni 1.08 hadi dola bilioni 1.03.