Feb 03, 2020 08:09 UTC
  • Magaidi waua raia 20 kaskazini mwa Burkina Faso

Afisa mmoja wa usalama nchini Burkina Faso amesema kuwa, raia wasiopungua 20 wameuawa katika shambulio la kigaidi lililotokea kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, magaidi wenye silaha wamekivamia kijiji cha Lamdamol kilichoko umbali wa takriban kilomita 40 kutoka mji wa Dori wa mkoa wa Seno wa kaskazini mwa Burkina Faso na kufanya umwagaji mkubwa wa damu. Magaidi hao walikuwa wamewalazimisha wanakijiji waondoke kijijini hapo, lakini wanakijiji walikataa hivyo jana Jumapili usiku magaidi wenye silaha waliwavamia na kufanya mauaji ya kikatili yaliyoua kwa umati wanavijiji 20.

Hali si shwari magharibi mwa Afrika

Hilo ni shambulio la pili la kikatili kufanywa na magaidi huko kaskazini mwa Burkina Faso. Tarehe 25 Januari pia nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ilikumbwa na shambulio jingine la kigaidi katika mkoa wa Sanmantonga na kuua raia 39. 

Kama zilivyo nchi nyingine za Mali na Niger, Burkina Faso nayo inashuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya magaidi kiasi kwamba tangu mwaka 2015 hadi hivi sasa watu 750 wameshauawa na zaidi ya 560 wamekimbia makazi yao.

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mwaka 2019 pekee, mashambulio ya kigaidi huko magharibi mwa Afrika yameua watu elfu nne wasio na hatia.

Tags