Zaidi ya watu 30 wapoteza maisha katika mafuriko nchini Sudan
-
Zaidi ya watu 30 wapoteza maisha katika mafuriko nchini Sudan
Mafuriko makubwa yamelikumba Jimbo la Nile nchini Sudan na kupelekea zaidi ya watu 30 kupoteza maisha na maelfu ya wengine kukwama kutokana na nyumba na maeneo yao kujaa maji ya mafuriko.
Maafisa wa kieneo wamesema kuwa, mafuriko ya mito ya Blue Nile na White Nile yameharibu mamia ya nyumba na kuzidisha mateso kwa wakazi wa maeneo hayo ambao tangu zamani walikuwa tayari wanaishi katika hali mbaya kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea Sudan hivi sasa.
Wakazi wa maeneo hayo wameelezea jinsi wanavyopitisha usiku mzima kwa hofu kubwa huku maji ya mafuriko yakikatiza katikati ya nyumba na mashamba yao.
"Tulishitukizwa na mafuriko," amesema Ramadhan Ali. "Tulikuwa tumelala yapata saa 7 na nusu usiku, wakati tulipovamiwa na mafuriko ghafla. Tuliamka, hatukuweza kupata njia ya kupambana na kiasi kikubwa mno cha maji. Kiasi cha maji ni kikubwa mno na hatukuweza kupambana nacho usiku huo wa manane. Lakini kwa sasa tunafanya kazi ya kuondoa maji. Hali yetu ni mbaya sana, nasisitiza, ni mbaya sana. Kwa kweli kila mtu hapa anateseka hivi sasa."
Ukosefu wa vifaa na zana umekawatisha tamaa wanaofanya juhudi za ndani za kupunguza uharibifu, huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha na kuzuia juhudi za uokoaji katika baadhi ya maeneo ya chi hiyo.
Majimbo mengine yaliyoathiriwa na mafuriko huko Sudan ni pamoja na Blue Nile, Al Jazirah na Khartoum. Katika jimbo la Mto Nile, wakazi wanasema kwamba janga hilo lingeweza kuepukwa kama hatua za mapema zingelichukuliwa na lau kama mamlaka husika zisingeliruhusu watu kujenga mazizi ya wanyama na maduka katika maeneo ambayo kawaida ndiyo yanayopitiwa na maji ya mafuriko.