Mahakama ya Afrika Kusini yatoa waranti ya kukamatwa Jacob Zuma
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58948-mahakama_ya_afrika_kusini_yatoa_waranti_ya_kukamatwa_jacob_zuma
Mahakama nchini Afrika Kusini imetoa waranti ya kukamatwa rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma anayeandamwa na kesi ya ufisadi katika mauzo ya silaha zilizokuwa na thamani ya dola bilioni mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 04, 2020 21:43 UTC
  • Mahakama ya Afrika Kusini yatoa waranti ya kukamatwa Jacob Zuma

Mahakama nchini Afrika Kusini imetoa waranti ya kukamatwa rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma anayeandamwa na kesi ya ufisadi katika mauzo ya silaha zilizokuwa na thamani ya dola bilioni mbili.

Jaji Dhaya Pillay alitangaza kutoa waranti dhidi ya Zuma jana Jumanne, baada ya rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini kukosa kufika mahakamani kwa kile kilichotajwa kama 'sababu za kiafya.'

Jaji huyo ametilia shaka barua ya daktari iliyowasilishwa mahakamani na wakili wa Zuma, Dan Mantsha ambaye anasema mwanasiasa huyo yuko nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. 

Ingawaje wakili wa Zuma hajaieleza mahakama kiongozi huyo anatibiwa katika nchi gani, lakini vyombo vya habari vya Afrika Kusini vimedai kuwa yuko nchini Cuba.

Zuma kizimbani

Kesi dhidi ya Zuma ilifutwa muda mfupi kabla ya kuwania nafasi ya urais mwaka 2009 lakini mashtaka hayo yalirejeshwa tena kortini baada ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kutangaza kuwa ina ushahidi wa kutosha wa kumshitaki.

Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini sasa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya rushwa baada ya mahakama kutupilia mbali ombi lake la kutaka kesi hiyo isitishwe kabisa.

Jaji Pillay amesema waranti dhidi ya Zuma itasalia kama ilivyo hadi kesi dhidi yake itakapoanza kusikilizwa tena Mei 6 mwaka huu.