Virusi vya Corona; watu 100 wawekwa karantini nchini Uganda
Wasafiri zaidi ya 100 wawekwa karantini baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege mjini Kampala nchini Uganda wakitokea nchini China.
Mamlaka ya Uwanja wa Ndege nchini Uganda imesema uamuzi huo umechukuliwa ili kuepusha hatari ya maambukizo ya virusi vya corona ambavyo husababisha maafa muda mfupi baada ya mtu kumbukizwa.
Waziri wa Afya wa Uganda, Dakta Jane Aceng amesema watu zaidi ya 100 kutoka nchini China wamewekwa kwenye karantini na watasalia katika hali hiyo ya kutengwa kwa muda wa siku 14 ili kufanyiwa uchunguzi wa kiafya katika hospitali na vituo mbalimbali vya kiafya nchini humo. Dakta Aceng ameongeza kuwa, miongoni mwa wasafiri hao waliotengwa ni raia 44 wa China.
Huku hayo yakiarifiwa, raia mmoja wa Argentina na mwengine wa China wanaoshukiwa kuwa na virusi hivyo wametengwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kiafya nchini Ghana.
Aghalabu ya nchi za bara la Afrika zimezidisha hatua za kiafya kwa ajili ya kukabiliana na maambukizo ya virusi hatarishi vya corona, huku jitihada zikiendelea ndani ya nje ya China kwa ajili ya kutafuta tiba ya ugonjwa unaosababishwa na virusi hivyo. Virusi hatari vya corona vilianza kujitokeza kwa mara ya kwanza mwezi Disemba mwaka jana 2019 katika mji wa Wuhan, mkoani Hubei nchini China na kuenea katika maeneo mengine ya dunia.
Hadi hivi sasa virusi hivyo vimeshaenea katika mikoa zaidi ya 30 ya China na nchi nyingine 18 duniani. Idadi ya walioaga dunia kwa virusi vya corona nchini China imeongezeka na kufikia 630.