Al Sisi atahadharisha kuhusu kupelekwa magaidi wa Syria katika nchi ya Libya
(last modified Sun, 09 Feb 2020 02:42:09 GMT )
Feb 09, 2020 02:42 UTC
  • Al Sisi atahadharisha kuhusu kupelekwa magaidi wa Syria katika nchi ya Libya

Rais wa Miisri ametahadharisha kuwa kuhamisha magaidi walioko Syria na kuwapelekwa Libya kutakuwa na matokeo hatari kwa nchi zote jirani za Kiafrika.

Abdel Fattah al Sisi ameliambia Baraza la Amani na Usalama la Afrika lililokutana kujadili mgogoro wa Libya kwamba, makubaliano ya kimataifa yaliyofikiwa Berlin nchini Ujerumani kuhusu Libya, yamekiukwa. Al Sisi ameongeza kuwa, amani haiwezi kupatikana nchini Libya hadi pale utajiri wa nchi hiyo utakapogawanywa kwa njia ya uadilifu.

Abdel Fattah al Sisi

Mkutano wa amani kuhusu Libya ulifanyika tarehe 19 Januari  katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin lengo kuu likiwa ni kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi na wawakilishi wa nchi 12, jumuiya 4 za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya nchi za Kiarabu. 

Maamuzi ya mkutano huo yalisisitiza udharura wa kuendelezwa vikwazo vya silaha dhidi ya Libya na kuzitaka nchi zote kuacha kuunga mkono na kusaidia upande wowote kati ya pande mbili hasimu. 

Baada ya kupinduliwa utawala wa Kanali Muammar Gaddafi huko Libya mwaka 2011, nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani na hivi sasa kuna serikali mbili hasimu, moja ya mashariki na nyingine ya magharibi mwa nchi hiyo ambapo vikosi vya pande hizo mbili vinaendelea kupigana,

Tokea Aprili mwaka jana wakati Haftar alipoanzisha vita dhidi ya mji mkuu Tripoli, watu wasiopungua 1,100 wameuawa, zaidi ya 5700 wamejeruhiwa na zaidi ya 146,000 kuachwa bila makao. 

Tags