Umoja wa Afrika wapinga Muamala wa Karne uliobuniwa na Marekani
Mkuu wa Kamisheni ya Afrika amesema kuwa, mpango wa Muamala wa Karne uko dhidi ya Wapalestina na unakinzana na sheria za kimataifa.
Moussa Faki aliyasema hayo jana Jumapili katika ufunguzi wa kikao cha viongozi wa Umoja wa Afrika nchini Ethiopia na kuongeza kuwa, mpango huo wa Marekani na utawala haramu wa Kizayuni, umetangazwa bila kuzingatia mitazamo ya upande wa Palestina na sheria za kimataifa. Aidha katika sehemu nyingine, mkuu huyo wa Kamishani ya Afrika ameashiria mauaji ya kila siku yanayofanywa dhidi ya watu wasio na hatia katika maeneo ya Pembe ya Afrika na ya Sahel ya bara hilo na kutaka zichukuliwe hatua za maana kwa ajili ya kuzuia maafa hayo ya kibinaadamu.
Umoja wa Afrika una wanachama 54 huku makao makuu yake ya kudumu yakiwa Addis Abab, Ethiopia. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mwanachama mtazamaji wa umoja huo. Rais Donald Trump wa Marekani akiwa pamoja na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel walizindua mpango huo walioupa jina la 'Muamala wa Karne' tarehe 28 Januari mwaka huu. Hata hivyo mpango huo umeendelea kupingwa katika kila pembe ya dunia.