Feb 11, 2020 12:54 UTC
  • Rais wa Tanzania amfuta kazi afisa wa serikali aliyeichana Qurani

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo, kuhakikisha anamuandikia barua ya kumfukuza kazi mfanyakazi wa wizara hiyo aliyechana na kuitemea mate Qurani Takatifu mkoani Morogoro.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Jumanne jijini Dar es Salaam, wakati akiwahutubia wananchi wa Kigamboni muda mfupi baada ya kuzindua rasmi Wilaya hiyo mpya na kusisitiza kuwa, serikali haipo tayari kuwa na wafanyakazi wapumbavu.

Amesema, “juzi nilikuwa namsikia Mheshimiwa Jafo, mtu mmoja kule Kilosa nafikiri alichana kitabu kitakatifu, nashukuru umechukua hatua ya kumsimamisha kazi. Lakini mimi namfukuza moja kwa moja, muandikieni barua ya kuondoka moja kwa moja."

Dakta Magufuli ameongeza kwa kusema, "ashinde kesi, asishinde huyo siyo mfanyakazi wa serikali. Hatuwezi tukakaa na wafanyakazi wapumbavu katika serikali hii. Umechukua jukumu la kumsimamisha kazi lakini mimi namfukuza."

Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro Wilbroad Mutafungwa alithibitisha hivi karibuni kukamatwa kwa afisa huyo wa wilaya aliyefahamika kwa jina la Daniel Maleki, kwa kosa la kuchana na kuchoma moto kitabu cha Juzuu Amma ambacho ni sehemu ya Quran Tukufu.

Qurani Tukufu

Alisema, “Maleki ni Afisa Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, alionekana akichana na kuchoma kitabu hicho Kitakatifu cha dini ya Kiislamu, kitendo ambacho kiliwakasirisha Waumini wa dini hiyo na wananchi waliokuwa maeneo hayo na kuamua kutoa taarifa kwa Polisi.”

Mahakama ilimnyima dhamana afisa huyo wa wilaya kwa misingi ya usalama wake, kwani nusra ashambuliwe na vijana wa Kiislamu walioghadhabishwa na kitendo hicho cha kukivunjia heshima kitabu chao kitukufu. Taasisi nyingi za kiraia nchini Tanzania likiwemo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania BAKWATA zimetoa taarifa za kulaani uafriti huo.

Tags