Kupingwa mpango wa Muamala wa Karne na viongozi wa Afrika
Tangu mpango wa Marekanii uliopewa jina la Muamala wa Karne ulipozinduliwa na Rais Donald Trump wa Marekani, mataifa na asasi mbalimbali za kieneo na kimataifa zimetangaza wazi kuupinga na kuukataa mpango huo na kuutaja kama mpango wa kidhalimu.
Upinzani wa walimwengu kwa Muamala wa Karne unatokana na ukweli huu kwamba, mpango huo umepuuza wazi wazi haki za taifa dhulumiwa la Palestina. Katika mwendelezo wa upinzani huo, viongozi wa Kiafrika walikutana hivi karibuni katika mkutano wao wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia ambapo pamoja na mambo mengine walitangaza kuupinga mpango huo na kuutaja kuwa usio wa kisheria.
Moussa Faki, Mkuu wa Kamisheni ya Afrika akihutubia katika kikao cha ufunguzi wa mkutano huo sambamba na kuashiria kwamba, mpango wa Muamala wa Karne unakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika na umeandaliwa bila ya kuzingatia mitazamo ya Wapalestina na sheria na kimataifa alisema: Mpango huu umeandaliwa bila ya mashauriano ya kimataifa na unazikanyaga haki za Wapalestina.
Kwa upande wake Rais Abdul-Fattah al-Sisi amesema kuwa, malengo matukufu ya Wapalestina daima yataendelea kubakia katika nyoyo na utajo wa wananchi wa Afrika.
Ikumbukwe kuwa, Jumanne ya tarehe 28 Januari, Rais wa Marekani, Donald Trump alizindua mpango wa Muamala wa Karne akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu.
Kuitambua rasmi Baitul-Muqaddas (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, kuupatia utawala huo haramu umiliki wa asilimi 30 ya eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kupingwa haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea nchini kwao na kupokonywa silaha kikamilifu ile itakayoitwa nchi ya Palestina ni miongoni mwa vipengele vya mpango huo wa udhalilishaji.
Hatua hiyo ya Trump ilikabiliwa na ingali inakabiliwa na malalamiko ya wananchi katika akthari ya mataifa ya dunia hususan kaskazuini mwa Afrika katika nchi kama Algeria, Morocco, Misri, Tunisia na hata huko Sudan.
Akihitubia katika mkutano wa Umoja wa Afrika, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye Jumapili iliyopita alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika amesema kuwa, mapendekezo ya Rais Donald Trump kwenye 'Muamala wa Karne' yanashabihiana na mfumo wa kipindi cha utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid) katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika na akatangaza kulaani mpango huo.
Wananchi wa nchi mbalimbali barani Afrika wamefanya maandamano na kuulaani mpango uliojaa njama wa Marekani wa Muamala wa Karne. Waandamanaji nchini Tunisia huko kaskazini mwa Afrika mbali na kupiga nara dhidi ya Marekani wameutaja Muamala wa Karne kama mpango mbaya na usiofaa.
Maandamano kama hayo yameshuhuudiwa pia katika nchi ya Morocco. Waandamanaji wenye hasira walijitokeza katika mji mkuu wa nchi hiyo Rabat ambapo mbali na kutangaza kuupinga na kuulaani mpango wa Muamala wa Karne wametoa wito wa kususiwa bidhaa za Marekani. Waandamanaji hao wakiwa wamebeba bendera za Palestina walisikika wakipiga nara za kuliunga mkono taifa la Palestina huku wengine wakiwa wamebeba maberamu yaliyoandikwa: Palestina Haiuzwi.
Nchini Sudan pia kumefanyika maandamano makubwa ya kupinga mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne. Waandamanji hao waalisikika wakipiga nara za kumlaani vikali Luteni Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan Kiongozi wa Baraza la Utawala la Sudan ambaye hivi karibuni alikutana na kufanya mazungumzo ya siri mjini Entebe, Uganda na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel. Aidha waandamanaji hao wametoa wito wa kuuzuliwa Abdul-Fattah al-Burhan na kueleza kwamba, wanapinga kwa nguvu zote hatua yoyote ile ya kutaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
Malalamiko dhidi ya mpango wa Muamala wa Karne yanaendelea kusuhudiwa katika nchi mbalimbali barani Afrika, katika hali ambayo, akthari ya viongozi wa nchi mbalimbali duniani pia wakiwemo wa Umoja wa Ulaya nao wameushutumu na kuulaani mpango huo.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, uzinduaji na uungaji mkono wa Trump kwa mpango huo bila shaka unathibitisha wazi kwamba, rais huyo wa Marekani ameazimia kuendeleza siasa zake za upande mmoja katika ngazi za kimataifa na kizitwisha nchi nyingine siasa hizo za mabavu.
Kwa hakika Marekani ambayo inajiona kuwa nguvu kubwa zaidi duniani inaendelea kupiga ngoma ya siasa za upande mmoja katika ngazi za kimataifa, katika hali ambayo nchi nyingi za dunia wakiwemo washirika wake wa Ulaya, haziipi tena umuhimu misimamo na matakwa ya serikali ya Donald Trump.