Watu wenye silaha waua kwa umati wanavijiji 20 katikati ya Mali
Maafisa wa serikali ya Mali wametangaza habari ya kuuawa kwa umati wanavijiji 20 baada ya watu wenye silaha kuvamia kijiji chao katikati ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Maafisa wa eneo hilo wamesema kuwa, watu wenye silaha Alkhamisi usiku walikivamia kijiji cha Ogossagou cha katikati ya Mali na kuua kwa umati watu wasiopungua 20. Wanamgambo wa kabila la Dogon ndio wanaotuhumiwa kufanya mauaji hayo.
Mkuu wa kijiji cha Ogossagou amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, wanamgambo wapatao 30 wamekivamia kijiji hicho baada ya jeshi la serikali kuondoka.
Mwezi Machi mwaka jana pia kijiji hicho kilishuhudia mauaji makubwa ya umati ambayo yalipelekea kuuliwa kwa halaiki watu 160 wa kabila la wafugaji la Fulani.

Licha ya jeshi la Mali kwa kushirikiana na askari wa kigeni kama wa Ufaransa kuchukua hatua mbalimbali, lakini bado nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika inaendelea kushuhudia machafuko na vitendo vya mara kwa mara vya kigaidi.
Huku hali ikiwa hivyo, jana iliripotiwa kuwa, jeshi la Mali limechukua udhibiti wa eneo la Kidal ambalo lilitekwa na waasi miaka sita iliyopita. Mji huo wa kaskazini mwa Mali ulikuwa unashikiliwa na waasi wa Tuareg wanaopigania kujitenga.
Taarifa zinasema kuwa, kikosi cha askari takribani 300 walioondoka katika mji wa Bamakao mapema Jumatatu wiki iliyopita na kuwasili katika mji huo wa kaskazini wa Mali wakiwa wanasindikizwa na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (MINUSMA). Hatua ya Jeshi la Mali ya kuchukua udhibiti wa Mkoa wa Kidali ni ishara ya ushindi kwa serikali ya Mali, ambayo inajitahidi kurejesha mamlaka yake katika eneo la Kaskazini.