Misri yapongeza kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Sudan Kusini
(last modified Mon, 24 Feb 2020 11:49:12 GMT )
Feb 24, 2020 11:49 UTC
  • Misri yapongeza kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Sudan Kusini

Serikali ya Misri imepngeza kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Sudan Kusini na kusema kuwa ina matumaini hatua hiyo itatoa fursa ya kushuhudiwa utulivu na usalama wa kudumu nchini humo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema hayo katika taarifa yake na kuongeza kwamba, Cairo itaendelea kuunga mkono juhudi za kuiletea amani ya kudumu Sudan Kusini kwa kushirikiana na waitifaki wake wa kieneo na kimataifa. 

Juzi Jumamosi, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hasimu wake mkubwa Riek Machar walitangaza kuunda serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ili kumaliza vita vya ndani nchini humo.

Kwa upande wake, Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Afrika (UNHCR) zimepongeza hatua ya kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na shauku kubwa huko Sudan Kusini.

Uundaji wa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa Sudan Kusini

 

Filippo Grandi, Kamishna wa UNHCR amesema katika taarifa kuwa, serikali mpya inahuisha matumaini ya amani na mustakabali mzuri kwa watu wa nchi hiyo ambao wameteseka kutokana na mgogoro wa muda mrefu.

Jumuiya ya IGAD imeahidi kuendelea kuiunga mkono serikali ya Juba ili kuhakikisha nchi hiyo changa zaidi barani Afrika inakuwa na amani ya kudumu, utulivu na ustawi. Umoja wa Afrika pia umepongeza kuundwa Serikali ya Umoja wa Kiataifa huko Sudan Kusini.

Hatimaye Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Sudan Kusini iliundwa juzi Jumamosi baada ya mkuu wa upinzani, Riek Machar kuapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Salva Kiir.

Tags