Serikali ya Misri: Ethiopia imeidhalilisha Jumuiya ya Nchi za Karabu
(last modified Mon, 09 Mar 2020 02:47:42 GMT )
Mar 09, 2020 02:47 UTC
  • Serikali ya Misri: Ethiopia imeidhalilisha Jumuiya ya Nchi za Karabu

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri imetangaza kuwa, inapinga vikali taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ethiopia kuhusu azimio la Baraza la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusiana na ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri imeeleza kuwa, bado kuna fursa ya kuweza kufikiwa makubaliano kuhusiana na kadhia ya Bwawa la al-Nahdha.

Kadhalika taarifa hiyo imeeleza kuwa, msimamo ulioatangazwa na Ethiopia si wa kidiplomasia na unaidhalilisha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Alkhamisi iliyopita nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiarabu ziliunga mkono msimamo wa Misri kuhusiana na mazungumzo yake na Ethiopia kuhusu Bwawa la al-Nahdha na kueleza kwamba, hatua yoyote ile ya upande mmoja itakayochukuliwa na Addis Ababa katika uwanja huo haikubaliki.

Ethiopia nayo ikatoa taarifa ikipinga msimamo huo wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Hivi karibuni Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ethiopia alikosoa nafasi ya Marekani katika kulitafutia ufumbuzi faili la ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha na kuitaja kuwa si ya kidiplomasia.

Ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha

Gedu Andargachew alisema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, pamoja na hayo nchi yake iko tayari kuendeleza na mazungumzo kuhusia na kadhia ya ujenzi wa Bwawa la al-Nahdha kwa upatanishi wa Marekani.

Bwawa la An-Nahdha linaendelea kujengwa juu ya Mto wa Blue Nile na katika eneo lenye urefu wa kilomita 40 katika mpaka wa pamoja wa Ethiopia na Sudan.

Serikali ya Misri inaamini kuwa asilimia 90 ya mahitaji ya maji ya nchi hiyo yanadhaminiwa na maji matamu ya Mto Nile na kwamba baada ya Bwawa la al-Nahdha kujazwa maji kikamilifu nchi hiyo itakabiliwa na matatizo makubwa ya uhaba wa maji. 

Tags