Watu 20 wauawa katika shambulizi dhidi ya kambi ya jeshi la Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59666-watu_20_wauawa_katika_shambulizi_dhidi_ya_kambi_ya_jeshi_la_uganda
Kwa akali watu 20 wameuawa katika shambulizi la wanamgambo waliobeba silaha dhidi ya kambi moja ya jeshi kaskazini magharibi mwa Uganda, mpakani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2020 00:26 UTC
  • Watu 20 wauawa katika shambulizi dhidi ya kambi ya jeshi la Uganda

Kwa akali watu 20 wameuawa katika shambulizi la wanamgambo waliobeba silaha dhidi ya kambi moja ya jeshi kaskazini magharibi mwa Uganda, mpakani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hayo yalisemwa jana Jumanne na Naibu Msemaji wa Jeshi la Uganda (UPDF), Luteni Kanali Deo Akiiki na kuongeza kuwa, askari watatu wa Uganda ni miongoni mwa watu 20 waliouawa katika shambulizi hilo dhidi ya kambi ya jeshi la nchi hiyo mnamo Machi 6 kaskazini mwa Bonde la Albertine, mpakani na Kongo DR.

Amesema wavamizi 80 wakiwemo waasi kadhaa wa DRC ndio waliotekeleza shambulizi hilo wakiwa wamebeba mapanga, mikuki na mishale, wakiwa na lengo la kuiba bunduki kambini hapo.

Kabla ya hapo, UPDF ilitangaza habari ya kuwatia mbaroni wapiganaji 25 kutoka kundi hilo linalotambuliwa na serikali ya Uganda kuwa la kigaidi karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ramani ya Uganda

Mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu, watu 30 waliuawa katika shambulizi la wanamgambo wa ADF huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo karibu na Uganda.

Katika miezi ya hivi karibuni, wanamgambo wa ADF ambao asili yao ni Uganda wamekuwa wakiwashambulia raia, maafisa usalama na hata maafisa wa afya wanaopambana na ugonjwa hatari wa Ebola, mashariki mwa Kongo DR na hata katika maeneo ya mpakani nchini Uganda.