Jeshi la Polisi Tanzania: Hatujawapiga wabunge wa upinzani
Jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam limetupilia mbali madai ya kuwapiga wabunge wa chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na kusisitiza kuwa, hilo sio jukumu lake.
Kauli hiyo imetolewa wakati chama hicho cha upinzani kikidai kuwa wabunge wake watatu wamelazwa hospitali ya Aga Khan baada ya kushambuliwa na polisi. Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, Zuberi Chembela amesema hakuna mwanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini humo aliyepigwa na jeshi hilo kwa kuwa hilo si jukumu lake. “Jukumu la polisi sio kupiga watu. Hao wanachama wa Chadema hawajapigwa na polisi labda waseme kuna waliowapiga lakini sio polisi." Amesema Chembela. Hii ni katika hali ambayo Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Demokrasia na Maendeleo Chadema, John Mrema amewataja wabunge hao kuwa ni Ester Bulaya, mbunge wa Bunda mjini, Halima Mdee, mbunge wa Kawe, Dar es Salaam na Jesca David Kishoa, mbunge wa Viti Maalum.
Kwa mujibu wa John Mrema, wabunge hao ni miongoni mwa watu takribani 27 waliokamatwa jana Ijumaa walipofika katika gereza la Segerea kumchukua mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyekuwa akitoka jela baada ya kukamilisha utaratibu wa kulipa faini ya Shilingi milioni 70. “Walipelekwa Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu kwa kuwa walikuwa na majeraha sana, wameumizwa. Tumetuma viongozi wetu wanafuatilia kwa sasa. Baada ya kupata taarifa ya hali zao tutawafahamisha.” Amesema Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema. Jana baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ilitangaza habari ya kujeruhiwa na polisi baadhi ya viongozi na wafuasi wa chama hicho cha upinzani wakati walipokwenda kumtoa gerezani Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Aikaeli Mbowe baada ya kukamilisha taratibu za kulipa faini mahakamani.