Kadhi Mkuu wa Kenya awakosoa wanaopuuza agizo la kutoenda misikitini
Kadhi Mkuu wa Kenya, Sheikh Ahmed Muhdhar amekosoa vikali hatua ya baadhi ya waumini wa Kiislamu ya kupuuza agizo la kuwataka wasiende misikitini kwa ajili ya Swala za jamaa katika kipindi hiki cha kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na kirusi cha Corona.
Sheikh Muhdhar ameonya kuwa, kupuuza agizo hilo katika kipindi hiki nyeti hakutakuwa na matokeo mengine ghairi ya kutahatarisha maisha ya waumini wa Kiislamu nchini humo.
Ameeleza bayana kuwa, "Qur'ani inatuagiza sisi Waislamu kumtii Allah, Mtume Wake na wenye mamlaka juu yetu. Tunapaswa kuswalia majumbani kwetu iwapo tumeagizwa kufanya hivyo. Kujaza misikiti hivi sasa kunahatarisha maisha yetu."
Hata hivyo amesisitiza kuwa, agizo hilo la kufungwa misikiti ni la muda, huku akiwataka Waislamu wote kumlilia Mwenyezi Mungu ili janga hili la corona limalizike.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Kamati ya Msikiti wa Jamia jijini Nairobi nchini Kenya, Abdul Bary Hamid alisema kwenye taarifa kuwa, hakutakuwa na mikusanyiko yoyote ya Swala za jamaa katika msikiti huo ambao ni mkubwa zaidi Afrika Mashariki, kwa muda usiojulikana.
Hamid alisema uamuzi huo uliafikiwa baada ya mashauriano baina ya usimamizi wa msikiti huo, Baraza la Majlis Ulamaa na Chama cha Madaktari Waislamu nchini Kenya (KAMMP). Misikiti kadhaa katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi na katika miji mingine ya Kenya imefungwa kutokana na hofu ya kuenea kirusi cha corona.