Kenya yazindua mpango wa kupima corona kwa watu wengi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60057-kenya_yazindua_mpango_wa_kupima_corona_kwa_watu_wengi
Wizara ya afya ya Kenya imeanza kufanya upimaji wa ugonjwa wa COVID-19 au corona kwa watu wote walioingia nchini humo wiki iliyopita na wale waliowekwa karantini kwenye vituo vya serikali au hoteli zilizoteuliwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 30, 2020 08:19 UTC
  • Kenya yazindua mpango wa kupima corona kwa watu wengi

Wizara ya afya ya Kenya imeanza kufanya upimaji wa ugonjwa wa COVID-19 au corona kwa watu wote walioingia nchini humo wiki iliyopita na wale waliowekwa karantini kwenye vituo vya serikali au hoteli zilizoteuliwa.

Waziri wa Afya wa Kenya, Mutahi Kagwe amesema, upimaji huo utafanyika kwa mujibu wa miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu upimaji wa corona, na kulingana na tarehe ya kuwasili kwao.

Kagwe pia amesema kutokana na hatari ya corona, na shinikizo kubwa kwa raslimali za huduma za afya, ni muhimu kwa serikali kuwalazimisha watu waliothibitika na wale waliokaribiana nao kuwekwa kwenye karantini.

Vilevile amewataka Wakenya kuzingatia usafi binafsi kwani ni msingi wa kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19. Hadi sasa watu 42 wameambukizwa corona nchini Kenya huku mtu mmoja akifariki na mwingine akipata nafuu.

Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe

Hadi sasa serikali ya Kenya imewapima watu 1,141 na miongoni mwao 163 wameruhusiwa kuenda nyumbani baada ya karantini ya siku 14 huku wengine 978 wakiendelea kufanyiwa uchunguzi baada ya kukutana na watu waliokuwa na corona.