Uganda yashtakiwa EACJ kwa 'sheria kandamizi' za kudhibiti corona
Wakili mmoja wa Uganda ameishtaki serikali ya Rais Yoweri Museveni katika Mahakama ya Uadilifu ya Afrika Mashariki EACJ akitaka kuondolewa zuio la kutoka nje lililotangazwa na serikali kama moja ya njia za kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 (corona) nchini humo.
Wakili huyo wa jijini Kampala, Wale Mabirizi amesema hatua hiyo ya serikali ya kudhibiti harakati na nyendo za watu si tu inakiuka katiba ya Uganda, bali pia inakanyaga Mkataba wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
Amesema maagizo ya kudhibiti maambukizi ya corona yaliyotolewa na Rais Museveni katika hotuba yake ya Machi 18 katika Ikulu ya Entebbe ni kinyume cha sheria.
Amesema maagizo hayo ya kufungwa shule na taasisi za elimu, misikiti, makanisa na maeneo mengine ya ibada, kuwazuia Waganda kusafiri nje ya nchi, na kuwalazimisha wasafiri kuwekwa karantini ya lazima kwa gharama zao wenyewe kwa muda wa siku 14 yanakiuka wazi wazi sheria za nchi.
Wakili Mabirizi amekosoa pia hatua ya Uganda kufunga mipaka ya nchi wanachama wa EAC, na kusisitiza kuwa mipaka hiyo inapawa kufunguliwa ili kuruhusu biashara miongoni mwa nchi wanachama kama ilivyoanishwa kwenye kanuni za Soko la Pamoja la jumuiya hiyo.
Wakati huo huo, Mawakili wa Haki za Binadamu wa Zimbabwe wameitaka Mahakama Kuu ya nchi hiyo kubatilisha agizo la kutotoka nje kwa lengo la kudhibiti corona, wakisisitiza kuwa maafisa wa usalama wametumia vibaya agizo hilo kuwahujumu raia wasio na hatia.
Mawakili hao wametaja kisa cha polisi wa Zimbabwe kumuachia mbwa wao na kumvamia mwanamke kwa jina Lucia Masvondo, 26, licha ya kuwa alikuwa katika boma lake akipika, kama moja ya mifano mingi ya ukiukaji wa haki unaofanywa na maafisa usalama wakati huu wa kutekeleza agizo la kutotoka nje nyakati za usiku.