HRW: Maafisa usalama wameua watu 31 nchini Burkina Faso
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60509-hrw_maafisa_usalama_wameua_watu_31_nchini_burkina_faso
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linawatuhumu maafisa usalama wa Burkina Faso kuwa wameua makumi ya watu waliowakamata katika operesheni zao dhidi ya makundi ya kigaidi.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Apr 21, 2020 03:25 UTC
  • HRW: Maafisa usalama wameua watu 31 nchini Burkina Faso

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linawatuhumu maafisa usalama wa Burkina Faso kuwa wameua makumi ya watu waliowakamata katika operesheni zao dhidi ya makundi ya kigaidi.

Corinne Dufka, Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika eneo la Sahel Afrika Magharibi alisema hayo jana Jumatatu na kuongeza kuwa, miili ya watu hao 31 waliouawa na maafisa usalama iligunduliwa mnamo Aprili 9 katika mji wa Djibo, kaskazini mwa nchi.

Mashuhuda 17 wameliambia shirika hilo kuwa, watu hao waliuawa muda mfupi baada ya kuchukuliwa kutoka majumbani mwao na maafisa usalama, na kwamba aghalabu yao ni watu wa kabila la Fulani. Mashuhuda wanasema miili ya wahanga hao ilikuwa imejaa matundu ya risasi.

Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika eneo la Sahel Afrika Magharibi amesema katika ripoti kuwa, "kitendo cha maafisa usalama kuua watu ambao hawajajizatiti kwa silaha ni cha fedheha na kinachotia doa operesheni za kupambana na magenge ya kigaidi."

Maafisa usalama wa Burkina Faso wanatuhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia katika operesheni zao

Ameitaka serikali ya Ougadougou kuchunguza tukio hilo na kuwafikisha mbele ya sheria waliotenda jinai hiyo, kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mbali na mamia kuuawa, zaidi ya watu elfu nne wanalazimika kuhama nyumba zao karibu kila siku nchini Burkina Faso kutokana na kuongezeka kiwango na idadi ya mashambulio yanayofanywa na makundi yanayobeba silaha dhidi ya raia wa nchi hiyo.