Libya kuongeza kiwango cha uzalishaji mafuta
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6061-libya_kuongeza_kiwango_cha_uzalishaji_mafuta
Viongozi wa Libya wamekubaliana na mpango wa awamu tatu wa shirika la taifa la mafuta la nchi hiyo wa kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu na kuufikisha katika kiwango cha kabla ya mwaka 2011.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 29, 2016 23:41 UTC
  • Libya kuongeza kiwango cha uzalishaji mafuta

Viongozi wa Libya wamekubaliana na mpango wa awamu tatu wa shirika la taifa la mafuta la nchi hiyo wa kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu na kuufikisha katika kiwango cha kabla ya mwaka 2011.

Shirika la taifa la mafuta la Libya lilisema jana (Ijumaa) kuwa lina matumaini - kwa uungaji mkono wa serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo - litaweza kurejesha kiwango cha uzalishaji mafuta nchini humo cha kabla ya kuanza kampeni za kumg'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi zilizoanza mwaka 2011.

Kiwango cha uzalishaji mafuta nchini Libya hivi sasa ni chini ya robo ya kiwango kilichokuwa kikizalishwa na Libya kabla ya kupinduliwa serikali ya Kanali Muammar Gaddafi. Wakati huo Libya ilikuwa ikizalisha karibu mapipa milioni moja na laki siku kwa siku.

Hata hivyo kurejesha kiwango cha uzalishaji mafuta cha kama ilivyokuwa katika kipindi cha serikali ya Muhammad Gaddafi ni jambo linalohitajia miaka mingi kwani hivi sasa kuna migomo ya mara kwa mara ya wafanyakazi wa taasisi za mafuta, kuna makundi kadhaa yenye silaha yanayodhibiti maeneo tofauti na hakujawa na serikali yenye nguvu ya kudhibiti kila kitu huko Libya.