Wanamgambo 89 wauawa Nigeria, mateka 5 wanusuriwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60611-wanamgambo_89_wauawa_nigeria_mateka_5_wanusuriwa
Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuwaangamiza makumi ya wanamgambo katika operesheni iliyofanyika katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 26, 2020 03:29 UTC
  • Wanamgambo 89 wauawa Nigeria, mateka 5 wanusuriwa

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuwaangamiza makumi ya wanamgambo katika operesheni iliyofanyika katika jimbo la Zamfara, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

John Enenche, msemaji wa jeshi la Nigeria alithibitisha habari hiyo hayo jana Jumamosi katika mahojiano na shirika la habari la Xinhua na kueleza kuwa,  "jumla ya wabeba bunduki 89 waliuawa katika operesheni ya vikosi vya jeshi siku ya Ijumaa katika mji wa Zurmi, huku mateka watano wakiwemo wanawake watatu na wanaume wawili wakiokolewa pia kwenye operesheni hiyo."

Amesisitiza kuwa, hakuna askari wa Nigeria aliyeuawa katika operesheni hiyo dhidi ya magaidi, na kwamba kubainisha kwamba wamefanikiwa kupata shehena ya silaha zilizokuwa mikononi mwa wanamgambo hao, mbali na ng'ombe 322 waliokuwa wameibwa, pikipiki 77, na simu za rununu tisa.

Msemaji wa Jeshi la Nigeria ameongeza kuwa, mpango wa kuwaunganisha mateka hao walionusuriwa toka mikononi mwa mgaidi na jamaa zao unaendelea.

Mapigano jimboni Zamfara

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya watu 47 kuuawa katika shambulio la majambazi wenye silaha dhidi ya vijiji kadhaa katika jimbo la Katsina, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Aidha mapema mwezi huu, watu 29 waliuawa katika shambulio la kigaidi dhidi ya maeneo mawili ya kaskazini na mashariki mwa Nigeria, mbali na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika yamekuwa yakikabiliwa na mashambulio ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram.