Wananchi wa Misri wahimiza kupambana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Syria
Harakati moja ya wananchi wa Misri imesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuishukuru Syria kwa kusimama kidete na kujitolea kupambana vilivyo na magenge ya kigaidi ambayo ni hatari kwa usalama wa dunia nzima, na imeyataka mataifa ya dunia kuungana kupinga vikwazo vya kidhulma vya Marekani dhidi ya Syria.
Hisham Lotfi, Mratibu Mkuu wa Kamati ya Mshikamano baina ya Wananchi wa Misri na Syria ameliambia shirika la habari la SANA kwamba serikali ya Marekani ambayo kwa miaka mingi inafanya njama dhidi ya Syria, sasa hivi imo katika kukamilisha njama zake hizo kupitia vikwazo vya kiuchumi dhidi ya wananchi wa Syria.
Ameongeza kuwa, kutokana na muqawama wake wa kupigiwa mfano, Syria imeweza kusimama imara kupambana na ugaidi na kuzibadilisha njama za kisiasa za kimataifa kuwa ushindi na lau kama si kujitolea huko taifa la Syria, basi ugaidi ungelienea dunia nzima. Hivyo ni wajibu kwa jamii ya kimataifa kukabiliana na mashinikizo ya upande mmoja ya Marekani dhidi ya nchi hiyo.
Tangu Syria ilipotumbukizwa kwenye mgogoro wa ndani mwaka 2011 hadi hivi sasa, Marekani iko mstari wa mbele kuyaunga mkono magenge ya kigaidi nchini humo kama ambavyo pia imeiwekea serikali ya Syria vikwazo vya kila namna licha ya kwamba Damascus imesimama imara kulinda usalama wa dunia nzima kupitia kupambana vilivyo na magenge ya kigaidi nchini humo.
Kwa upande wao, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, Shirika la Afya Duniani (WHO) na shirika la UNHCR wote wamekuwa wakihimiza kufutwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Syria hasa wakati huu wa maambukizi ya kirusi cha corona, lakini Donald Trump na serikali yake huko Marekani wanaendelea kung'ang'ania vikwazo hivyo.