Algeria: Hamaki za wengine hazitotufanya tuvunje uhusiano wetu na China
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60969-algeria_hamaki_za_wengine_hazitotufanya_tuvunje_uhusiano_wetu_na_china
Msemaji wa Ikulu ya Algeria amesema kuwa, uhusiano wa nchi yake na China ni mzuri, uko wazi na ni wa kipekee, hivyo hamaki za wengine haziishughulishi Algiers na itaendeleza uhusiano wake huo na China kama kawaida.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 14, 2020 03:22 UTC
  • Algeria: Hamaki za wengine hazitotufanya tuvunje uhusiano wetu na China

Msemaji wa Ikulu ya Algeria amesema kuwa, uhusiano wa nchi yake na China ni mzuri, uko wazi na ni wa kipekee, hivyo hamaki za wengine haziishughulishi Algiers na itaendeleza uhusiano wake huo na China kama kawaida.

Televisheni ya Rusia al Yaum imetangaza habari hiyo na kumnukuu msemaji wa Ikulu ya Algeria akisema hayo na kuongeza kuwa, uhusiano wa kipekee baina ya nchi yake na China umekuwepo tangu enzi taifa la Algeria lilipokuwa kwenye mapambano ya ukombozi ya kumtimua mkoloni Ufaransa. Wakati huo China iliiunga mkono kikamilifu Algeria na hadi leo hii inaendelea kuiunga mkono nchi hiyo katika matukio mbalimbali na ndio maana Algeria nayo iliiunga mkono China kupata kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Msemaji huyo wa Ikulu ya Algeria ameongeza kuwa, hamaki za baadhi ya watu haziwashughulishi na si muhimu kwao na kwamba siasa za mambo ya nje za Algeria ziko wazi katika jambo hilo.

Vile vile amesema, Rais Abdelmadjid Tebboune wa nchi hiyo anaupa umuhimu mkubwa uhusiano wa Algeria na nchi nyingine.

Itakumbukwa kuwa, Ufaransa ambayo iliwahi kuikoloni Algeria, imehamakishwa mno na misaada ya China kwa Algeria kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya kirusi cha corona.

Waalgeria wamesema, hamaki hizo za dola la kikoloni la Ulaya yaani Ufaransa, haziwashughulishi hata kidogo.