Washambuliaji wapanda-pikipiki wenye silaha waua watu 60 kaskazini mwa Nigeria
Watu 60 Wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa katika shambulizi lililofanywa na kundi la wapanda pikipiki wenye silaha kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Duru za habari nchini Nigeria zimeripoti kwamba kundi hilo likiwa na pikipiki karibu 100 lilivamia vijiji vya Aduwa, Kuzari, Kutama na Masawa katika jimbo la Sokoto, kaskazini magharibi mwa Nigeria. Mashuhuda wamesema kuwa wabeba silaha hao waliwashambulia kiholela wakazi wa vijiji hivyo sambamba na kuharibu mazao yao na kuwasababishia hasara kubwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mamia ya wakazi wa vijiji hivyo wamelazimika kuzikimbia nyumba zao kwa ajili ya kuokoa maisha yao. Tangu mwezi Mei mwaka jana majimbo saba ya kaskazini magharibi mwa Nigeria yamepiga marufuku matumizi ya pikipiki kutokana na vyombo hivyo vya usafiri kutumiwa vibaya na makundi ya kigaidi katika kutekeleza hujuma zao nchini humo.