Nigeria yalegeza sheria za kudhibiti corona, yafungua misikiti
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61444-nigeria_yalegeza_sheria_za_kudhibiti_corona_yafungua_misikiti
Nigeria imeanza kuondoa zuio na kulegeza sheria kali ilizokuwa imeweka kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19 ulioua mamia ya watu nchi humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 06, 2020 03:32 UTC
  • Nigeria yalegeza sheria za kudhibiti corona, yafungua misikiti

Nigeria imeanza kuondoa zuio na kulegeza sheria kali ilizokuwa imeweka kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19 ulioua mamia ya watu nchi humo.

Kwa mara kwanza baada ya wiki kumi, waumini wa Kiislamu katika mji mkuu Abuja jana walishiriki Sala ya Ijumaa katika misikiti mbalimbali ya jiji hilo. Waumini walipimwa kiwango cha joto la mwili kabla ya kuruhusiwa kuingia misikitini, huku wakilazimika kuchunga sheria ya mtagusano wa kijamii.

Hata hivyo shule na viwanja vya ndege vimeendelea kufungwa nchini Nigeria. Tangu lilipoanza wimbi la maambukizi ya corona hadi hivi sasa, Nigeria imeweka sheria kali za kukabiliana na ugonjwa huo ulioenea dunia nzima.

Hadi kufikia sasa, nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ilikuwa imenakili kesi zaidi ya 11,500 za watu walioambukizwa ugonjwa hatari wa COVID-19 ambapo watu zaidi ya 300 wameshafariki dunia.

Aghalabu ya nchi za Afrika zimeanza kulegeza sheria za kukabili maambukizi ya corona

Licha ya kesi za ugonjwa wa COVID-19 kuendelea kuongezeka barani Afrika, lakini akthari za nchi za bara hilo ama zimelegeza au zimeazimia kulegeza zuio na sheria za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Tunisia hivi karibuni pia ilifikia uamuzi wa kufungua mipaka yake ili kuokoa sekta ya utalii. Mipaka ya ardhini, angani na majini ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika inatarajiwa kufunguliwa Julai 27.