Watu 10 wauawa katika shambulizi la silaha nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61633-watu_10_wauawa_katika_shambulizi_la_silaha_nchini_nigeria
Kwa akali watu 10 wamepoteza maisha baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia vijiji katika jimbo la Benue, kaskazini mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 16, 2020 03:42 UTC
  • Watu 10 wauawa katika shambulizi la silaha nchini Nigeria

Kwa akali watu 10 wamepoteza maisha baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia vijiji katika jimbo la Benue, kaskazini mwa Nigeria.

Usman Suleiman, Mkuu wa Wilaya ya Agatu, amesema watu wasiojulikana walishambulia wakulima waliokuwa wakirejea nyumbani kutoka shambani, na kwamba watu 10 wamepoteza maisha huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika shambulizi hilo.

Amesema kuwa majeruhi wamelazwa hospitalini, na kuwa vikosi vya usalama vimepelekwa katika eneo hilo kwenda kudhibiti hali. Ameongeza kuwa, uchunguzi rasmi umeanzishwa ili kuwabaini wahusika wa shambulio hilo na malengo yao.

Hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo, ingawaje genge la Boko Haram limekuwa likitekeleza hujuma za namna hii huko nchini Nigeria.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya raia zaidi ya 40 na wanajeshi wasiopungua 20 kuuawa katika mashambulizi mawili tofauti huko kaskazini mashariki mwa Nigeria. Mashambulizi hayo yalijiri katika maeneo ya Monguno na Nganzai katika jimbo la Borno Jumamosi iliyopita.

Wanachama wa Boko Haram

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilianza kufanya hujuma zake za silaha mwaka 2009 kwa lengo la kujiimarisha huko kaskazini mwa Nigeria. 

Katika kipindi chote hicho, watu zaidi ya elfu 20 wameuliwa katika mashambulizi ya magaidi wa Boko Haram huko Nigeria, Cameroon, Niger na Chad; na wengine zaidi ya milioni mbili wamekuwa wakimbizi.